RAIS DKT. SAMIA ASISITIZA UMUHIMU WA ELIMU KWA WATOTO WA KIKE,MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA PROGRAMU YA MWANAMKE KIONGOZI
Na Mwandishi wetu,DmNewsOnline
DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanawake waliobahatika kupata fursa ya elimu na kuwa viongozi kwenye maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kuongeza imani na amani kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanza kwa Mafunzo ya ongozi kwa Wanawake Tanzania (Female Future Program) sambamba na Mahafali ya Wahitimu wa Awamu ya 10 ya Mafunzo hayo na Mkutano wa 7 wa Uongozi, yaliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka wahitimu hao kuwa chachu ya maendeleo katika jamii na kutumia elimu na stadi za ongozi walizopata kunufaisha jamii kwa ujumla.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amewarai wanawake kudhihirisha ushupavu wa uongozi kwenye Mashirika na Taasisi mbalimbali na kuwataka kuwa wabunifu kwenye kazi zao na kuwa waaminifu katika kulipa kodi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya mwananchi.
Pia, katika kuhakikisha ustawi wa jamii, Rais Dkt. Samia amewahusia kuwa pamoja na elimu na nafasi za ongozi walizonazo, wasiache wajibu wao wa kijamii wa malezi na makuzi ya watoto ili kuwaepusha kujiingiza kwenye mienendo isiyofaa.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dkt. Samia amewahamasisha wanawake wenye sifa na uwezo
kujiandikisha kupiga kura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba-Doran, amesema wastani wa wahitimu kila mwaka umekuwa na washiriki 45, huku awamu ya tatu ikiwa na idadi ndogo zaidi (21) kutokana na athari za UVIKO-19, na Awamu ya Kumi ikiwa na washiriki wengi zaidi (110) ingawa mwenendo wa ushiriki umekuwa ukipanda na kushuka.
Ameongeza kuwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko maradufu: 2015 (36), 2016 (30), 2017 (21), 2018 (30), 2019 (36), 2020 (36), 2021 (44), 2022 (77), 2023 (73), na 2024 (110) ambapo mpaka sasa ambapo kuna jumla ya washiriki 493 kutoka sekta binafsi na sekta ya umma wamepata mafunzo hayo.










Comments
Post a Comment