‎ATE YAZINDUA RASMI MUHULA WA 11 YA PROGRAMU YA MWANAMKE KIONGOZI " FEMALE FUTURE PROGRAMME " ‎

Na Mwandishi wetu,MwelekeoMediaOnline

‎Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha ESAMI, Peter Kiuluku, ametoa wito kwa wanafunzi wa Programu ya Mwanamke Kiongozi kufuatilia na kujifunza kutoka kwa viongozi wa juu wa serikali, akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kupata mwongozo wa kuwa viongozi bora katika sekta mbalimbali.
‎Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa muhula wa 11 wa programu hiyo, inayoendeshwa kwa ushirikiano wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Chuo cha ESAMI, na washirika kutoka Norway, Kiuluku amesema Dkt. Samia ameendelea kuwa kielelezo cha uongozi bora unaochochea maendeleo.
‎“Viongozi hujifunza kutoka kwa wengine, na kuwa na mifano mizuri ya kuigwa ni muhimu kwa uimarishaji wa uongozi wenye tija,” amesema Kiuluku.
‎Ameeleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa wanawake kupata mafunzo haya, kwani wanawakilisha zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya watu nchini.
‎“Iwapo kuna idadi kubwa ya wanawake katika jamii, ni muhimu pia kuwashirikisha katika uongozi. Ushirikiano wa wanawake na wanaume katika nafasi za uongozi utasaidia kuendeleza nchi na taasisi zetu,” ameongeza.
‎Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzzan Ndomba, amesema Programu ya Mwanamke Kiongozi si ya Tanzania pekee, bali inatekelezwa pia katika nchi nyingine tano za Afrika, ikiwemo Kenya, Uganda, Ghana, Tunisia, na Jordan.
‎“Washiriki wa programu hii watajiunga na mtandao mkubwa wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Norway, ambako programu hii ilianzishwa,” amesema Ndomba.
‎Amebainisha kuwa programu hiyo inajumuisha masomo matatu makuu—uongozi, mawasiliano, na umahiri katika bodi—ikiwa na lengo la kuwajengea wanawake ujuzi wa kuongoza na kuongeza uwakilishi wao katika ngazi mbalimbali za uongozi.
‎“Kama Chama cha Waajiri, tunasimamia masuala ya waajiri nchini, na mojawapo ya malengo yetu ni kuhakikisha usawa wa kijinsia katika sehemu za kazi. Programu ya Mwanamke Kiongozi ni sehemu ya jitihada hizo,” ameongeza.
‎Ndomba amesema kuwa mpaka sasa, programu hiyo imeleta mabadiliko chanya katika sehemu za kazi, huku idadi ya kampuni zinazoshiriki ikiongezeka kila mwaka.



Comments

Popular posts from this blog

MAHAFALI YA COHORT YA 11 YA MWANAMKE KIONGOZI, SPIKA ATOA MATUMAINI MAPYA USAWA WA KIJINSIA

‎Wingu Africa appoints Prasad Acharya as Director of Sales for Tanzania ‎

ACCELERATED ENTRY : HOW EAST AFRICA LEAPFROGGED INTO THE CLOUD AGE