‎WAJIRI WATAKIWA KUWEKEZA KATIKA AFYA NA USTAWI WA WAFANYAKAZI ‎




Na Mwandishi wetu, Mwelekeomedia 

‎NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Evalline Munis amewataka waajiri nchini kuweka malengo yanayopimika ya afya na ustawi wa wafanyakazi katika mipango yao ya kila mwaka ili kuhakikisha uwekezaji katika afya unaleta matokeo yanayoonekana katika kuongeza tija, ubunifu na ushindani wa biashara.
‎
‎Ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika bonanza la tano la afya la waajiri lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kuongozwa na kauli mbiu isemayo Wekeza kwenye afya, fungua fursa kwa mafanikio zaidi limewakutanisha waajiri, wafanyakazi na wadau mbalimbali kwa ajili ya michezo, uchunguzi wa afya na elimu kuhusu ustawi mahala pa kazi.
‎
‎Amesema waajiri wanapaswa kuifanya afya kuwa sehemu ya mikakati ya biashara zao badala ya kuichukulia kama jambo la msimu, kwa kuwekeza katika uchunguzi wa afya wa mara kwa mara, kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili na mazingira salama yanayohamasisha wafanyakazi kufanya mazoezi.
‎
‎Aidha amesisitiza kuwa wafanyakazi wenye afya bora na ari ya kazi huchangia kuongeza ubora wa kazi, ubunifu na huduma kwa wateja, huku uwekezaji katika ustawi wao ukisaidia kupunguza utoro, ajali na gharama zinazotokana na matibabu pamoja na kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi.
‎

‎Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa chama cha waajiri Tanzania- ATE, Suzan Ndomba, amesema chama hicho kinaendelea kushirikiana na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kutoa elimu kwa waajiri kuhusu umuhimu wa kulinda afya za wafanyakazi, akisisitiza kuwa hakuna tija bila afya bora mahala pa kazi.
‎
‎Aidha ameeleza kwamba bonanza hilo lilianzishwa miaka mitano iliyopita kwa lengo la kuwakutanisha waajiri na wadau mbalimbali, kuwajengea uelewa kuhusu afya na usalama mahala pa kazi, pamoja na kuimarisha mahusiano kupitia shughuli za pamoja, ikiwemo mazoezi ya viungo.
‎ 





Comments

Popular posts from this blog

A scientific breakthrough in malaria is only the beginning ‎

COMMUNITY ACTION IS KEY TO REDUCING MALARIA IN TANZANIA ‎

‎Wingu Africa appoints Prasad Acharya as Director of Sales for Tanzania ‎